Wednesday, 16 May 2018

ELIMU MFUMO WA ULIPAJI KODI PANGO LA ARDHI KIELEKTRONIKI YATOLEWA.

Na. Maua Patrick.
ELIMU imeendelea kutolewa ili kuhakikisha mfumo huu wa ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kielektroniki unakuwa na tija.
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeanzisha mpango wa kutoa mafunzo kwa kuteua kikosi kazi kinachotoa mafunzo juu ya matumizi ya mfumo huo.
Hatua hiyo imefikiwa ili kuelimisha mikoa mingine baada ya kupata mafanikio mazuri katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi.
Miongoni mwa njia kuu na muhimu kwa nchi kujipatia maendeleo ni kuzingatia ulipaji wa Kodi.
Serikali imezingatia suala hili kwa kuboresha mifumo ya ukusanyaji malipo mbalimbali  malipo ya ndani.


 
.   OfisakutokaWizarayaArdhi, Nyumba naMaendeleo ya Makazi Haruna Kiyungi, akieleza jinsi ya kutumia Mfumo waulipa kodi ya pango la ardhi kwanjia ya kielektroniki.

Kwa hatua ya kwanza ilizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato wa Serikali kwa njia ya kielektroniki (e-RCS), uliotengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa kutumia wataalamu wa ndani.

Akizindua mfumo huo katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu (NIDC), kilichopo Kijitonyama, Rais Dk. John Magufuli, alisema   “Wanaokusanya mapato wanalalamika kuwepo kwa udanganyifu kwenye utoaji taarifa za wafanyabiashara.
Ofisa Ardhi David Malisa (katikati) akitoa mafunzo kwa Maofisa kutoka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi kanda ya Ziwa jinsi ya kutumia Mfumo wa GePG.

Wafanyabiashara nao wanalalamika kubambikizwa kodi, sasa dawa ya haya yote yatatatuliwa na uwepo wa kituo hiki, jiungeni na mfumo huu kwani kila kitu kinafanywa na mashine, hakuna kuonea mtu,”.
Kwa maana hiyo, serikali imeamua kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli kuwa wa kielektroniki, ili kurahisisha ukusanyaji wake na kuongeza uwazi miongoni mwa wizara na taasisi mbalimbali za serikali.
Aidha, kwa upande wa malipo ya kodi ya pango la ardhi, dhana ya ulipaji wa kodi hiyo inatokana na Sheria ya Ardhi namba 4, ya mwaka 1999, fungu la 3, kifungu kidogo cha 1(a).
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, zimedhamiria kuboresha malipo ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa ‘GePG’.
Mfumo huo utahusika katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na tozo zingine zinazotokana na sekta ya ardhi nchini.
Hivi karibuni mfumo wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya simu ya mkononi  umeanza kutumika Wizara ya Ardhi kwa makusanyo ya pango la ardhi.
Mfumo huo, unawarahisishia mwananchi kulipia popote alipo kwa kutumia tovuti ya wizara au simu za mkononi kwa wananchi wanaomiliki viwanja au mashamba yaliyopimwa.
Watapatiwa hati maalum ili ku ataweza kutumia simu yake ya mkononi kuona kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na kulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi Dk. Moses Kusiluka, anazungumzia utaratibu wa mapato ya kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kielektroniki na kueleza uamuzi wa kufunga akaunti za kukusanyia kodi hii, kupisha mfumo mpya.
Dk. Kusiluka anawatahadharisha wamiliki wa ardhi wenye hati au hati maalumu ijulikanayo kwa jina la ‘ofa’, kuhakikisha wanalipa kodi hiyo kwa wakati, vinginevyo muda wa malipo ukipita watatozwa faini ambayo wasipolipa  baada ya siku 14 watapelekwa mahakamani.
Anasema ili mwananchi kujua anadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi kwa kutumia simu ya mkononi, anatakiwa kubonyeza *152*00# kuandika ujumbe na kutuma kwenda namba 15200.
Baada ya hapo anaweza kulipia kwa njia ya mitandao ya simu na benki.
Anaeleza huduma zingine za sekta ya ardhi, zinazohusisha malipo hayo ni tozo mbalimbali za sekta ya ardhi ikiwemo upekuzi katika daftari la msajili, ambapo mwananchi atapaswa kutembelea ofisi za wizara zilizopo katika eneo lake.
Baada ya hapo atapatiwa makadirio ya kulipia huduma husika pamoja na namba ya malipo itakayomuwezesha kulipia kwa njia ya benki na simu ya mkononi.
Kwa mmiliki wa ardhi iliyopimwa na kupatiwa hati ya umiliki, Kaimu Katibu Mkuu huyo anasema anaweza kuulizia kiasi cha fedha anayodaiwa na kulipia kodi husika.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dk. Shaaban Pazi, anabainisha kwamba mfumo wa GePG, ulianza kutumika rasmi Juni, mwaka huu.
“Mafunzo ya awali yalitolewa kwa ofisi ya Dar es Salaam na maeneo mengine, mfumo huu ni rafiki kwani utaboresha na kurahisisha ukusanyaji wa malipo ya kodi ya pango la ardhi.
Mkurugenzi  wa mifumo ya kifedha Wizara ya Fedha na Mipango, John Sausi, anasema njia ya ulipaji wa kodi hiyo kwa mtandao utaiongezea serikali makusanyo ya kodi kwa wakati.
“Kutokana na makusanyo hayo kwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya serikali, itaondoa msongamano wa watu waliokuwa kwenye utaratibu wa awali wa ulipaji kodi.
Uanzishwaji wa mfumo huo utaenda sawia na utoaji elimu ya matumizi kwa wananchi ili waweze kujihudumia kwa haraka na uhakika,” anasema.
.  Maofisa kutoka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa wakijifunza jinsi y akutumia mfumo huo.

Halima Chitemi, mkazi wa Dar es Salaam,  akiwa katika foleni ya kufanya malipo ya kodi hiyo wizarani, baada ya shighuli ya utoaji elimu, hakuwa tayari kuanza kufanya malipo hayo kwa njia ya simu akihofia kutofanikiwa kukamilisha malipo hayo.
Hata hivyo Adam Manase, ambaye akiwa kwenye foleni hiyo, alikubali kufanya malipo hayo kupitia simu yake na kufanikiwa vema huku akiwaacha waliohofia kutumia njia hiyo wakisubiri kwenye foleni.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dennis Masami, anawahamasisha wananchi kutambua mabadiliko ya utaratibu wa ulipaji kodi hiyo.
Badala ya watu kufika wizarani kwa ajili ya kufanya malipo ya kodi ya pango la ardhi, hivi sasa wafanye kwa nija ya kielektroniki.
 “Kwanza mtu ataweza kufanya makadirio ya madeni yake kwa njia ya simu au kupitia tovuti ya serikali na kulipia kwa njia ya mtandao au benki husika jambo litakalosaidia kuokoa muda,” anasema.
Masami anaeleza licha ya mfumo wa kielektroniki kurahisisha ulipaji wa kodi hiyo, pi utawezesha malipo kufanyika kwa usalama zaidi na kuzuia mianya ya utapeli.
Changamoto kadhaa zimejitokeza ambazo wizara imebaini na inaendelea kuzifanyia kazi ikiwemo kundi la watu wasioweza kufanya malipo hayo kwa kutomiliki simu na kukosa  huduma ya mtandao katika maeneo yao.
“Wizara inaandaa utaratibu wa kusajili vipande vyote vya ardhi ili wamiliki wote wa ardhi ya mijini ambao hawajasajiliwa, wasajiliwe ili wahusike kulipa kodi hiyo.
Pia lipo kundi la wamiliki wa ardhi kadhaa wanaofanya malipo hayo kielektroniki na kuhitaji risiti za karatasi, zaidi ya zinazopatikanika kwenye simu ambapo hulazimika kufika kwenye ofisi ya halmashauri husika,” anasema.
Anasema ujenzi wa kituo cha mfumo wa kielektroniki wa kumbukumbu za ardhi  umeanza kutekelezwa, ukikamilika utaboresha uwekaji wa kumbukumbu za wamiliki wa ardhi na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa kodi za ardhi kwa ubora zaidi.
Ujenzi wa jengo la kituo cha mfumo wa kielektroniki wa kumbukumbu au uhifadhi wa taarifa za ardhi, kwa sasa umekamilika na kitajulikana kwa jina la ‘Kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi’.
Ni matumaini wizara itazingatia weledi katika ukusanyaji wa kodi ambazo kimsingi zitatumika kuleta maenbdeleo ya taifa.
Pia elimu zaidi iendelee kutolewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa ulipaji kodi na matumizi ya njia ya kielektroniki.
000


0 comments:

Post a Comment